Sunday, 8 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alihudhuria Mahafali ya Saba ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar yaliyofanyika Tunguu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiyapoke maandamano ya Wahitimu wa Mahafali ya Saba ya Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar yaliyofanyika kwenye viunga vya chuo hicho kiliopo Tunguu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.

Wahitimu wa ngazi ya Stashahada wa Chuo cha Utawala wa Umma wakivaa kofia kuashiria kutunukiwa stashjahada zao baada ya kuhitimu mafunzo yao happ Tunguu nje kidogo ya Mji wa Zanzibar. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ. 
Mmoja wa wahitimu wa chuo cha Utawala wa Umma  waliofanya vyema kwenye mafunzo yao akikabidhiwa tuzo kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif ambae ndie mgeni rasmi katika Mahafali ya saba ya Chuo hicho. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ. 

Balozi Seif akizungumza na wahitimu wa ngazi ya Cheti na Stashahada wa Chuo cha Utawala wa Umma kwenye mahafali ya saba ya chuop hicho hapo Tunguu.  Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akikata Keki Maalum iliyotayarishwa na Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma kunogesha sherehe hizom zilizofanyika katika viwanja vya chuo hicho vilivyopo Tunguu Wilaya ya Kati. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
Baadhi ya Wahitimu wa Chuo cha Utawala wa Umma wakionyesha furaha yao wakiwa katika mahafali ya kumalizia mafunzo yao ya cheti na Stashahada. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.

 Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema ili kupata utumishi wenye tija ni lazima kwa kila mtumishi kufanya kazi kwa kujituma zaidi, ubunifu pamoja na kujiamini na asione tabu kupata ushauri kutoka kwa mwenzake pale anapokwama.
Alisema ili kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya ulimwenguni inayotokana na kukuwa na sayansi na teknoloji hakuna budi watumishi kubadilika na kubadilisha mfumo wa utendaji kazi.
Akizungumza kwenye mahafali ya saba ya chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar yaliyofanyika kwenye chuo hicho Tunguu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar ambapo alipata fursa ya kutunuku vyeti na Stashahada kwa wahitimu wa chuo hicho  Balozi  Seif alisema wakati wa kufanya kazi kwa mazoea hivi sasa umekwisha na kupitwa na wakati.
Jumla ya wahitimu elfu 1,402 wa fani  14 zikiwemo mbili mpya za Mahusiano ya Kimataifa na Diploma pamoja na Uhazili yametolewa chuoni hapa kwa mwaka 2013/2014 katika ngazi ya cheti na Stashahada.
 Balozi Seif Ali Iddi alieleza ni vyema watumishi wote wakahakikisha kwamba wanautumia vyema muda wao wa kazi kwa maendeleo ya Taifa vyenginevyo ni kulisababishia Taifa hili kuachwa nyuma wakati mengine yakisonga mbele.
Alitoa wito kwa wahitimu wote hasa wale waliomo ndani ya utumishi wa Umma na wanaotarajiwa kuingia katika utumishi huo wanaitumia vilivyo taalum waliyoipata katika mchakato wa mageuzi ya Utumishi wa Umma.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alielezea mafaja yake kuona chuo cha utumishi wa umma kinaratibu na kutoa mafunzo  ya awali { Induction Course } kwa watumishi wapya wa umma wanaoajiriwa ili kuwapa uelewa wa maadili, miiko na taratibu za kiutumishi.
Alisema mafunzoi hayo ni muhimu kwa vijana wapya kwa vile jamii imekuwa ikishuhudia matukio mengi ya uvunjaji wa maadili ya kazi hasa kwa vijana wapya wanaoingia katika utumishi wa umma.
Balozi Seif aliutaka uongozi wa Chuo hicho kujikita zaidi katika kuandaa mafunzo mafupi ya kujenga uwezo kwa watumishi na watendaji wa ngazi tofauti yakiwemo mafunzo ya Uongozi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa.
Alieleza kwambia si vibaya wakatumia uzoefu wa vyuo nyengine ndani na nje hya nchi katika kupata uzoefu wa jinsi Taasisi na vyuo hivyo vinavyoandaa na kuendesha mafunzo mbali mbali.
“ Wenzetu hawa wamepiga hatua kubwa katika mageuzi ya utumishi, hatuna budi nasi kuendelea kujifunza kutoka kwao. Jaribuni kuwa na uhusiano wa karibu na vyuo hivyo, ikiwezekana hata kubadilishana wanafunzi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akizungumzia suala la Utafiti Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza umuhimu wa chuo hicho  kujikita katika kufanya tafiti mbali mbali katika utumishi wa Umma.
Alisema ni hatua nzuri kwa Chuo Cha Utawala wa Umma kuandaa rasimu ya mapendekezo ya kufanya utafiti ikiwemo maswali ya ushibiti wa taka, lakini ni vyema tafiti zao zikalenga kwenye maswali ya ufanisi kazini.
Balozi Seif alifafanua kwamba Zanzibar na Tanzania kwa ujumla zina wasomi wengi lakini ni wachache kati yao wanaojishaghulisha kufanya utafiti pamoja na kuandika.
Alisema  mambo mengi yanagunduliwa kutokana na mchangfo wa matokeao ya tafiti mbali mbali  zinazosababisha kupatikana kwa maendeleo ya taasisi pamoja na Taifa kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alilipongeza Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma kwa usimamizi wake katika harakati za ujenzi wa majengo mapya yanayoendeshwa na chuo chenyewe.
Alisema ujenzi huo ni mafanikio ya kupigiwa mfano ambapo kukamilika kwake kutatoa fursa kwa chuo kupanua wigo wa shughuli zake ikiwemo kutoa mafunzo ya viwango vya juu zaidi.
Aliuhakikishia Uongozi wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kadri ya hali ya kifedha itakavyoruhusu kuunga mkono juhudi za chuo katika kuendeleza ujenzi huo.
Akisoma Risala ya wahitimu hao wa chuo cha Utawala wa Umma mwanafunzi Mbarouk Kheir Othman alisema kwamba chuo hicho ni sekta muhimu inayozalisha rasilmali watu ambayo hufanikisha ustawi wa utumishi wa Taifa.
Mbarouk Kheir aliiomba Serikali iendelee kuwekeza katika elimu ambayo ndio msingi wa ufanisi katika maisha ya kila mwana jamii, taasisi za umma au Serikali kwa ujumla.
Alisisitiza umuhimu wa Jamii kujikita katika kukiunga mkono chuo cha Utawla wa Umma  kinachozalisha mbegu ya rasilmali watu na kuongeza ufanisi wa uwajibikaji katika Taasisi za Umma.
Mapema Mkurugenzi wa Chuo cha Utawala wa Umma Bibi Arusi Masheko Ali alisema chuo hicho kiko katika maandalizi ya kutoa mafunzo ya Ujasiri Amali kwa Watumishi wanaostaafu katika Taasisi za Umma na zile Binafsi ili kuwajengea msingi imara wa kuendelea kujiendesha kimaisha mara wamalizapo Utumishi wao.
Bibi Arusi alisema maandalizi hayo yako  katika hatua nzuri kwa Uongozi wa Chuo hicho kwa Kushirikiana na Taasisi inayosimamia maslahi ya wastaafu ambao ni Mfuko wa ufihadhi wa Jamii Zanzibar { ZSSF } Itakayoratibu mafunzo hayo.
Mkurugenzi huyo wa Chuo cha Utawala wa Umma alifahamisha kwamba Uongozi wa chuo hicho unaendelea na juhudi za  kutafuta fursa zaidi za masomo kwa walimu wa Chuo hicho ili kuwajengea uwezo wa ufundishaji unaokwenda na wakati walimu hao.
Bibi Mahseko aidha alitoa wito kwa watumishi, wanafunzi na wananachi wa Kisiwa cha Pemba kulitumia Tawi la Chuo cha Utawala wa Umma lililofunguliwa kIsiwani humo.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi Balozi Seif kuzungumza na Wahitimu hao wa Chuo cha Utawala wa Umma Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utawala wa Umma Mh. Haroun Ali Suleiman waliwashukuru Walimu wa Chuo hicho kwa kazi kubwa waliyoifanya ambayo imeleta mabadiliko makubwa ya kiutendaji chuoni hapo.
Waziri Haroun alisema juhudi za walimu hao zinafafana na zile zilizochukuliwa na Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Taasisi za ndani na nje ya Nchi za kusimamia uanzishwaji wa elimu ya Juu na hivi sasa Zanzibar tayari ina vyuo vikuu Vitatu.
Aliwahakikishia walimu na wanafunzi wa elimu ya Sekondari Zanzibar kwamba Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Kazi na Utawala wa Umma utasimamia ipasavyo juhudi za kuanzishwa na kiwango cha Shahada katika Chuoi cha Utawala wa Umma Zanzibar.
Chuo cha Utawala wa Umma Zanzibar kiliopo Tunguu Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar kimekuwa kikitoa mafunzo katika ngazi ya Cheti na Stashahada katika fani za Usimamizi wa Rasilmali Watu,Utawala wa Umma, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano pamoja na Mahusiano ya Uma.
Fani nyengine ni Mahusiano ya Kimataifa na Diplomasia, Ununuzi wa Ugavi,Utunzaji wa kumbu kumbu na Nyaraka pamoja na  Uhazili.