Wednesday, 11 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifajiri Familia ya Sheha wa Shehia wa Kibweni

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiifajiri Familia ya Sheha wa Shehia wa Kibweni Bibi Asha Ali Nassor ambayo moja ya chumba cha nyumba hiyo kimeteketea na kuunguza vitu vyote vilivyokuwemo. Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Mohammed Mahmoud. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akikagua hasara iliyotokana na moto katika chumba cha Nyumba ya Sheha wa Kibweni Bibi Asha Ali Nassor Wilaya na Magharibi Mkoa wa Mjini Magharibi.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud na kulia ya Balozi Seif ni Mmoja wa miongoni mwa wakaazi wa Nyumba hiyo Bwana Abdulla Kombo Hamad. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.





















Mtoto wa Sheha wa Shehia ya Kibweni anayeishi ndani ya chumba kilichoteketea kwa Moto Bibi Asumini Moh’d Juma akimueleza Balozi Seif mkasa ulimpata kutokana na maafa hayo ya moto. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.

  Press Release:-
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewashukuru na kuwapongeza Wananchi wa Mtaa wa Kibweni  Wilaya ya Magharibi kwa moyo wao waliouonyesha katika kusaidia kuuzima moto ulioibuka majira ya saab 7.00 usiku juzi kwenye nyumba ya Sheha wa Shehia ya Kibweni Bibi Asha Ali Nassor.
Alisema licha ya kwamba vitu vyote vilivyokuwemo ndani ya chumba cha mmoja wa watoto wa Sheha huyo alitwae Asumini Moh’d Juma kuteketea kwa moto huo lakini juhudi za pamoja kati ya wakaazi wa nyumba hiyo na wananchi jirani zimesaidia kuepuka maafa zaidi katika janga hilo.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati alipofika Kibweni kuwafariji wakaazi wa nyumba hiyo na kuwapa mkono wa pole kutokana na maafa hayo akiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Magharibi Nd. Ayoub Moh’d Mahmoud.
Alishauri na kuomba mpango huo uendelezwe zaidi ili kutoa faraja kwa wananchi wanaopatwa na maafa katika matukio mbali mbali yakiwemo yale ya moto na hata ya tabia nchi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtaka mpatwa na maafa hayo Bibi Asumini Moh’d  Juma kuwa na moyo wa subira katika kipindi hichi cha  mtihani na kumtakia hali ya utulivu katika maisha yake ya baadaye.
Mapema Mmmoja wa mashuhuda ya tukio hilo anayeishi ndani ya nyumba hiyo Abdulla Kombo Hamad alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba  moshi mkubwa uliotanda ndani ya nyumba hiyo ndio chanzo kilichowatanabahisha kuwepo kwa hali isiyo ya kawaida vyumbani humo.
Abdullah  Kombo alisema wakazi wa nyumba hiyo kwa kusaidiana na majirani walilazimika kuvunja mlango wa Chumba kilichokuwa na moshi mwingi cha Bibi Asumini ambaye kwa wakati huo alikuwa Harusini na kufanikiwa kuuzima moto huo.
Alifahamisha kwamba baada ya kuangalia kwa kina chanzo cha moto huo walichodhania kuwa ni hitilafu za umeme, wakagundua  kuwa ni chupa ya mafuta ya Petroli iliyopenyezwa kwenye durisha la nyuma la chumba hicho.
Abdullah  Kombo Hamad alielezea faraja yake baada ya kuona juhudi zao pamoja na majirani  zilisaidia kuudhibiti moto huo usiathiri mfumo wa waya za umeme zilizomo ndani ya nyumba hiyo.
Naye Mkaazi wa chumba hicho Bibi Asumini Moh’d Juma alisema kwamba moto huo umesababisha kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa vimehifadhiwa  ndani ya chumba chake.
Bibi Asumini alivitaja baadhi ya vitu vilivyokuwemo ndani ya chumba chake kuwa  ni pamoja na kabati lililohifadhiwa nguo zote, Kitanda na Godoro lake,Charahani, vyakula pamoja na baadhi ya vitu vya ndani.
Alisema licha ya mtihani huo lakini anawashukuru watu wa wasamaria mbali mbali kwa moyo wao wa huruma waliomuonyesha wa kumpatia baadhi ya huduma zikiwemo nguo za kujistiri hali iliyompa faraja kubwa.