Monday, 23 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi Kikundi cha Mazoezi ya Viungo cha Upendo chenye Maskani yake katika Kijiji cha Uzini ndani ya Wilaya ya Kati.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikata utepe kuashiria kuyaruhusu maandamano ya wana mazoezi ya viungo wa vikundi mbali mbali walioshiriki uzinduzi wa IKikundi cha Upendo cha Uzini kuingia ndani ya viwanja vya michezo vya skuli ya Uzini. Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Dr. Idriss Muslim Hijja na kushoto yake ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii jna Michezo Said Ali Mbarouk. Picha Hassan Issa  - OMPR –ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akikizindua rasmi Kikundi cha mazoezi ya viungo cha Upendo chenye maskani yake katika Kijiji cha Uzini Mkoa wa Kusini Unguja. Picha Hassan Issa  - OMPR –ZNZ.
Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Moh’d Raza Hassanali hakua nyuma katika kuungana na wanamichezo wa vikundi vya Mazoezi wakati wa uzinduzi  wa kikundi cha Upendo Uzini kiliomo ndani ya Jimbo analoliongoza. Picha Hassan Issa  - OMPR –ZNZ.
Baadhi ya vikundi rafiki vya mazoezi hapa Unguja vilivyoshiriki kwenye uzinduzi wa Kikundi cha Mazoezi cha Upendo cha Kijiji cha Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. Picha Hassan Issa  - OMPR –ZNZ.

Vijana wadogo wa Kikundi cha mazoezi cha Nurl - jana cha Mtaa wa Magogoni wakifanya vitu vyao wakati wa mazoezi ya uzinduzi wa Kikunci cha Upendo cha Uzini.
Picha Hassan Issa  - OMPR –ZNZ.





















Uzee sio sababu ya kutofanya mazoezi. Hivyo ndivyo inavyoonekana kwa Mzee Salum Abeid wa pili kutoka kulia kutoka Kikundi cha Mazoezi ya Viungo cha Upendo Uzini akionyesha mfano huo bila ya kupumzika hadi mwisho wa zoezi.

 Picha Hassan Issa  - OMPR –ZNZ.

  Press Release:-


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa mara nyengine tena ndani ya saa 24  amekizindua rasmi Kikundi cha Mazoezi ya Viungo cha Upendo chenye Maskani yake katika Kijiji cha Uzini ndani ya Wilaya ya Kati.
Uzinduzi huo ameufanya katika viwanja vya michezo vya Skuli ya Sekondari Uzini  na kushirikisha pia vikundi mbali mbali vya Zoni “D” pamoja na vile vikundi rafiki vya mazoezi viliopo hapa Unguja.
Balozi Seif Ali Iddi aliyaongoza maandamano ya wana vikundi walioshiriki  katika uzindui huo yaliyoanzaia  Kijiji cha Mgeni Haji Kibombani hadi Skuli ya Uzini akiambatana na Viongozi wa Wizara ya habari, Utamaduni, Utalii na Michezo pamoja na wa Serikali wa Wilaya ya Kati na Mkoa wa Kusini Unguja.  
Akizungumza na wanavikundi hao Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wananchi lazima watenge muda maalum katika kufanya uchunguzi wa afya  zao licha ya kufanya mazoezi ya kila siku.
Balozi Seif alisema wapo watu miongoni mwa Jamii wanaotembea na kuendelea na harakati zao za kimaisha kila siku bila kujitambua kwamba wamezongwa na  matatizo ya kiafya.
Alisema mazonge kama hayo ndio chanzo kikuu kinachowasababishia watu wa aina hiyo kupata vifo vya ghafla na kuwaacha jamaa na watu wa karibu kushangaa na kuanza dhana na  shutuma ya kumtafuta mbaya wake.
“ Jamaa na marafiki wanabakia kushangaa na kuanza  shutuma kwamba mwenzetu huyu  si bure kwa hili  hapa upo mkono wa mtu “. Balozi Seif alisema hizo ni fikra potovu zinazoweza kuleta mfarakano ndani ya familia na jamii kwa ujumla.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kuwakumbusha wanamichezo na wananchi wote kuendeleza amani na utulivu uliopo hapa Nchini na kuwakemea wale wanaoshika bango la kutaka kuzusha balaa la kuiharibu amani hiyo.
Alifahamisha kwamba Jamii itahamanika na kutawanyika bila ya kujali athari itayowakumba akina mama na watoto endapo hali ya amani na utulivu itapotea hapa nchini.
“ Sisi tunataka kuendelea kufanya mazoezi yetu na kuishi bila ya vurugu. Sasa wale wenzetu wanaosimamia bango la kutaka kuzua balaa ya kuiharibu amani yetu lazima inatupasa tuwakemee kwa nguvu zetu zote “ Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikipongeza Kikundi cha mazoezi ya Viungo cha Upendo cha Uzini na kuahidi kwamba zile changamoto zinazokikabili kikundi hicho hasa suala la vifaa vya kusaidia Jamii katika usafi wa mazingira atalichukulia hatua za haraka.
Mapema Daktari wa kitengo cha kudhibiti maradhi yasiyoambukiz Dr. Omar Abdulla alisema zaidi ya asilimia 33% ya maradhi ya moyo na asilimia 3% ya maradhi ya Kisukari ya watu hapa Zanzibar wameathirika na magonjwa hayo.
Dr. Omar alisema chanzo cha ongezeko la maradhi hayo hapa Nchini kinatokana na watu kutopenda kufanya mazoezi sambamba na kutumia kwa kiwango kikubwa vyakula vya mafuta.
 Mchango wa papo kwa papo ulifanywa katika hafla ya uzinduzi wa Kikundi cha Upendo Uzini kwa lengo la kusaidia kuimarisha kikundi hicho kilichoanzishwa karibu miaka Mitatu iliopita.
Zaidi ya shilingi Milioni 3,000,000 zimepatikana katika mchango huo ulioongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiwa kinara wa kuunga mkono wachangiaji mbali mbali waliojitokeza wakiwemo Viongozi wa Serikali.