Monday, 16 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akionya Uongozi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali Amana Kisiwani Pemba kuwapimia Viwanja Wananchi katika eneo la Kifoi Wete.

 Afisa mdhanini Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Said Iddi Hamad wa pili kutoka kulia akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliyepo Kushoto kuhusu uamuzi wa Wizara hiyo wa kuwapimia Viwanja Wananchi katika eneo la Kifoi Wete ambalo limeleta mzozo na Kamisheni ya Wakfu Kisiwani Pemba. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
 Balozi Seif akikata Sabuni ya Mchi kuangalia ubora wake wakati alipoutembelea ushirika wa akina Mama wa kutengeneza sabuni za Miti na za kukogea wa Miti Ulaya Wete Kisiwani Pemba akishuhudia wa wanaushirika huo kulia yake. Nyuma ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mheshimiwa Omar Khamis Othman. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ






















Mshika fedha wa Ushirika wa akina mama wa kutengeneza sabuni za Miti na za kukogea wa Miti Ulaya Wete Kisiwani Pemba Bibi Maryam Rashid Moh’d akimuonyesha Balozi Seif Kidumu cha Sabuni za Kuogea wanazozalisha kwenye kiwanda chao. Wa mwanzo kushoto ni Mwanachama wa Ushirika huo wa Selem Women Center Miti Ulaya Wete Bibi Naima Abdulla. Picha na Hassan Issa – OMPR – ZNZ.

   Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuonya Uongozi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali Amana Kisiwani Pemba kusitisha mara moja zoezi la uwekaji wa Mabango  ya kuzuia ujenzi wa Nyumba katika eneo la ardhi lenye mzozo liliopo Kifoi – Limbani Wete pamoja na lile la Junguni Gando Kisiwani Pemba.
Amesema iwapo Uongozi huo wa Wakfu na Mali ya Amana ulikuwa ukitekeleza agizo uliyopewa na Kiongozi yeyote yule suala hilo litajadiliwa katika Vikao vya Baraza la Mapinduzi Zanzibar hapo baadaye.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo alip[ofanya ziara fupi kukagua eneo hilo ambalo limekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Kamisheni ya Wakfu na wananchi waliopewa viwanja na mamlaka husika kujenga nyumba za kuishi.
Alisema eneo hilo la Kifoi Limbani Wete Pemba ni miongoni mwa Maeneo ambayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyagawa kwa Wananchi eka tatu tatu mara tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ili waendeleze shughuli za Kilimo.
Alifahamisha kwamba Hati zote zilizotolewa na kutumika kuhusu umiliki wa matumizi ya Ardhi katika Visiwa vya Zanzibar kabla ya mwaka 1964 hazitumiki tena na kwa sasa ni batili.
Balozi Seif alisisitiza kwamba ardhi yote ya Visiwa vya Zanzibar ni mali ya Serikali. Hivyo alisema mipango yoyote itakayoamuliwa na Serikali katika matumizi ya ardhi hiyo popote pale ndani ya Zanzibar ni lazima iheshimiwe na Wananchi pamoja na Taasisi ziwe za umma na hata binafsi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikemea kwamba kitendo cha Uongozi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali Amana Pemba kuendesha zoezi la uwekaji wa Mabango ya kuzuia ujenzi linaweza kuamsha chuki, uhasama na hatimae kusababisha vurugu za kuvunja amani.
“ Naagiza kwamba zoezi la Wakfu na Mali ya Amana lisimame mara moja na mabango yote yaliyowekwa yang’olewe. Nikimaliza vikao vya Baraza la Wawakilishi Unguja vinavyoendelea hivi sasa nitafanya ziara ya kuja kungalia kama agizo langu limetekelezwa “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliuasa Uongozi huo wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Pemba kwamba hauna idhini ya kuzuia Mashamba yaliyogawa Serikali eka tatu tatu kwa Wananchi mwaka 1964 bali wanachokifanya ni uamuzi wa Watu binafsi na kamwe hilo ni jambo lisilokubalika.
Akitoa ufafanuzi  Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Ndugu Said Iddi Hamad alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wizara hiyo kupitia Idara ya Ardhi na Mipango Miji ilikata viwanja na kugaia Wananchi kwa lengo la kujenga nyumba za Kuishi.
Nd. Said alisema hatua hiyo imekuja baada ya eneo hilo kuanza kuvamiwa na kuanzishwa ujenzi holela jambo ambalo Taasisi ya Ardhi  ikalazimika kuchukuwa hatua za kitaalamu za kulipima eneo hilo katika mfumo unazingatia mipango miji.
Mapema Sheha wa Shehia ya Limbani Bwana Masoud Ali Hassan alisema kwamba eneo hilo la Kifoi – Limbani Wete limegaiwa kwa Wananchi Eka Tatu tatu maara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 19664.
Sheha Masoud alisema shughuli za ujenzi  wa makaazi ya nyumba za kudumu ndani ya eneo hilo ulianza zaidi ya miaka 20 baada ya Mapinduzi  kukiwa hakuna malalamiko wala madai dhidi ya wahusika hao.
Alisema anashangaa kuona Uongozi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Kisiwani humo ukiendesha zoezi la uwekaji wa mabango ya kuzuia ujenzi au shughuli zozote katika kipindi hichi ukidai kwamba hiyo ni shmba na Wakfu ya Marehemu Bwana Abdullah Bin Suleiman El – Busaid wa Limbani Wete.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman alieleza masikitiko yake dhidi ya Uongozi wa Taasisi hiyo ya Wakfu Pemba kwa kuchukuwa hatua za uendeshaji wa zoezi hilo bila ya kuiarifu Serikali ya Wilaya ya Wete wala ile ya Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Mh. Omar alisema Uongozi huo ulichukuwa uamuzi huo bila ya kuzingatia kwamba maeneo wanayoyapima hivi sasa yanatumiwa na wananchi kwa kazi na shughuli mbali mbali za  kilimo pamoja na ujenzi.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikitembelea kikundi cha Ushirika wa Akina Mama cha Utengenezaji wa Sabuni za Michi na kukogea cha Miti Ulaya Mjini Wete.
Akizungumza na wana ushirika hao Balozi Seif aliwataka akina mama hao kuendelea kuzingatia  vyema maadili na taratibu zilizowekwa kuhusu uendeshaji wa vikundi vya ushirika.
Alisema vipo vikundi vingi vilivyoanzishwa hapa nchini na kuanza vyema shughuli zao za uzalishaji lakini vikashindwa kudumu kutokana na baadhi ya wanachama wake hasa wale viongozi waliopewa dhamana kukosa maadili.
Akizungumzia suala la uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi oktoba mwaka huu Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wana ushirika hao ni vyema wakawalinganisha mapema viongozi wenye nia safi ya kukubali kuwatumikia.
“Baadhi ya waheshimiwa wamekuwa na tabia zinazofanana na simu ya mkononi.  Wakeshaichaji hawana habari tena na wale waliowachagua. Hivi sasa wameanza kutafuta waya wa kuchajia kwa sababu uchaguzi umekaribia “. Balozi Seif aliwatahadharisha akina mama hao.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi na wana ushirika wa Utengenezaji wa Sabuni za Michi na kukogea Miti Ulaya Wete kwa uwekaji wa kumbu kumbu za matumizi na kuahidi kuwalipia deni lao wanalodaiwa katika shughuli za ujenzi wa Jengo lao la kudumu.
Mapema Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi aliwataka akina mama hao kujituma zaidi katika miradi yao ya kuiuchumi na maendeleo kwani wao ndio walezi wakuu wa familia.
Mama Asha alisema hayo hayata patikana wala kufanikiwa iwapo akina mama hao kwa kushirikiana pamoja na akina bab hawatadumisha Umoja, Mshikamano na upendo miongoni mwao.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika kuunga mkono juhudi za akina Mama hao wa Kiwanda cha utengenezaji wa Sabuni za michi na kuogea aliahidi kukichangia shilingi Milioni 3,000,000/- ili zisaidie kupunguza changamoto zinazowakabili ikiwemo baadhi ya vifaa na mali ghafi za mradi wao.