Monday, 16 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa agizo kwa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Zanzibar kuufutia hati ya matumizi ya ardhi Mfuko wa kuhudumia Watoto yatima Zanzibar.

 Eneo la Mawe Mazito la Hecta 20 liliopo Vitongoji  chake chake Pemba ndilo pekee lilopbakia Kisiwani humo kwa ajili ya upatikanaji wa rasimlali ya jiwe kwa ujenzi wa miundombinu ya bara bara. Picha Hassan Issa– OMPR – ZNZ.
 Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Hemed Salum wa pili kutoka kulia akimpatia maelezo Balozi Seif aliyefika kukagua eneo la mawe mazito ambalo liko chini ya dhamana ya Mfuko wa Kuwahudumia Watoto Yatima Zanzibar Hapo Vitongoji Chake chake Pemba. Wa kwanza kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mh. Mwanjuuma Majid na Mwakilishi wa Kampuni ya Mecco Bwana Abdullkadir Moh’d Bujeti. Picha Hassan Issa– OMPR – ZNZ.






















Mwakilishi wa Kampuni ya ujenzi wa Miundombinu ya Bara bara ya Mecco Bwana Abdullkadir Moh’d Bujeti akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hatua iliyofikiwa ya kukamilika kwa ujenzi wa Bara bara Tatu zaMkoa wa Kaskazini Pemba. Picha Hassan Issa– OMPR – ZNZ.

Press  Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametoa agizo kwa Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Zanzibar kuufutia hati ya matumizi ya ardhi Mfuko wa kuhudumia Watoto yatima Zanzibar { Zanzibar Children Fund } iliyopewa katika eneo la mawe mazito liliopo Vitongoji Chake chake Pemba.
Alisema eneo hilo la Hekta 20 ndilo pekee lililobakia Kisiwani Pemba linalotumiwa na Wizara ya Miundo mbinu na Mawasiliano kwa ung’oaji wa mawe mazito yanayotumiwa katika miundo mbinu ya ujenzi wa mawasiliano ya Bara bara.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua eneo la Mawe mazito na kuiagiza Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati kufanya utaratibu mara moja wa kuupatia sehemu nyengine Mfuko huo ili uendelee na malengo yake iliyojipangia.
Alisema uamuzi huo wa Serikali umekuja baada ya eneo la Hekta 133 lililotengwa na Serikali kwa ajili ya shughuli ya uchimbaji mawe mazito Kisiwani Pemba kumalizika kwa rasilmali hiyo muhimu kwa ujenzi wa miundo mbinu ya bara bara.
“ Nitamuagiza Waziri anayehusika na masuala ya Ardhi aifute hati iliyopewa Mfuko wa kuhudumia Watoto Zanzibar na badala yake awapatie sehemu nyengine ili kupisha eneo hilo litumiwe kwa kazi nyengine za uchimbaji wa mawe mazito kwa ajili ya uimarishaji wa miundombinu ya Bara bara “. Alisema Balozi Seif.
Alisema utafiti wa Kitaalamu uliofanywa na wataalamu wa Mazingira na mali zisizorejesheka umebaini kwamba eneo hilo la Vitongoji walilopewa Mfuko huo ndio sehemu pekee iliyobaki ndani ya Kisiwa cha Pemba yenye mali ghafi yam awe mazito.
“Hii sehemu ndio pekee iliyobaki kuwa na jiwe gumu linalofaa kwa ujenzi wa Bara bara. Hivyo italazimika hati iliyopo kufutwa na litumike kwa kazi nyengine za Serikali “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba Ardhi ni Rasilmali ya Taifa. Hivyo Serikali wakati wote ina haki na wajibu wa kulitumia eneo la Ardhi popote pale Nchini kwa maslami ya Jamii nzima.
Alieleza kwamba ipo faraja kidogo kwa Serikali kulitumia eneo hilo hivi sasa kwa vile halijawa na mali nyingi ya mmiliki wa matumizi isipokuwa jengo moja tuu ambapo ingelazimika kulipa fidia.
Mapema Afisa Mdhamini Wizara ya Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Hemed Salum alisema kwamba eneo hilo la Hecta 20 za ardhi walizopewa Mfuko huo wa Kuhudumia Watoto Yatima Zanzibar ni miongoni mwa Hekta 133 zilizotengwa maalum ya Serikali kwa kazi ya uchimbaji wa Mawe mazito.
Nd. Hemed alisema Mfuko wa Kuhudumia Yatima Pemba waliomba eneo hilo kwa ajili ya kujenga Kijiji cha Mayatima Karibu miaka sita sasa tokea mwaka 2009 akini hadi sasa eneo hilo bado halijaekezwa kitu chochote zaidi ya ujenzi wa jengo moja.
Eneo  pekee lenye rasilmali ya jiwe zilo linalofaa kwa matumizi ya miundombinu ya mawasiliano ya Bara bara Kisiwani Pemba kwa sasa lipo Vitongoji karubu Kilomita nne Mashariki mwa Mji wa Chake chake Pemba.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alipata wasaa wa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bara bara ya Wete Gando na Gando Ukunjwi unaosimamiwa na Kampuni ya Mecco.
Mwakilishi wa Kampuni ya Mecco Bwana Abdullkadir Moh'Bujeti alimueleza Balozi Seif kwamba wahandisi wa ujenzi wa Bara bara hiyo wanaendelea na harakati za ujenzi katika kiwango cha kuridhisha.
Bwana Bujeti alisema kazi iliyobakia katika ujenzi wa Bara bara ya Wete Gando hivi sasa ni ya kukamilisha Kilomita 3.6 na ile ya Gando Ukunwi imebakisha Kilomita 2.
Alifahamisha kwamba kazi kubwa iliyobakia kwa sasa katika mradi huo ni uwekaji wa alama za bara barani pamoja na rangi na baadaye kukabidhiwa Rasmi Serikalini mwishoni mwa Mwezi wa Machi Mwaka huu wa 2015.
Akitoa shukrani zake kwa hatua kubwa iliyofikiwa na Kampuni ya Mecco katika kukamilisha mradi huo wa ujenzi wa Bara bara sita za Kisiwa cha Pemba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alielezea kuridhika kwake na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa bara bara hizo.
Balozi  Seif alisema kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ya Bara bara Kisiwani Pemba kutatoa fursa pana kwa wananchi hasa wakulima Kisiwani humo kuwa na uwezo wa kusafirisha mazao yao  kwa uhakika kupelekea kwenye soko.