Tuesday, 24 March 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitia saini Mkataba wa uendelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Micheweni

Afisa Uendeshaji Tiba Kisiwani Pemba Bwana Ali Moh’d Mbarawa  mwenye karatasi mkononi akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyevaa suti ya buluu juu ya Ujenzi wa Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Micheweni kabla utiaji saini Mkataba wa uendelezaji wa ujenzi huo.Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
Muonekano wa Jengo litakalokuwa Kituo cha upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba linalotarajiwa kugharimi jumla ya shilingi Milioni 340,000,000/- litakapokamilika. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.
Kaimu Balozi wa Japan Nchini Tanzania Bwana Kazuyoshi Matsunaga akiwa pamoja na Afisa Uendeshaji Tiba Kisiwani Pemba Bwana Ali Moh’d Mbarawa wakitia saini Mkataba wa ujenzi wa Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Micheweni.
Utiaji saini huo umeshuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa tatu kutoka Kulia, Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dr. Saleh Mohammed Jidawi kushoto yake na Mkuu wa Wilaya ya Wete Nd. Hassan Khatib Hassan.Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman, Katibu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Jimbo la Konde Nd. Ismail Juma na Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Nd. Jabu Khamis Mbwana. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.

Kaimu Balozi wa Japan Nchini Tanzania Bwana Kazuyoshi Matsunaga akibadilishana mawazo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa jengo la Upasuaji la Hospitali ta Wilaya ya Micheweni Kisiwani Pemba.
Kulia ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mheshimiwa Omar Khamis Othman. Picha Hassan Issa –OMPR – ZNZ.




















Kaimu Balozi wa Japan Nchini Tanzania Bwana Kazuyoshi Matsunaga akisisitiza msimamo wa Serikali yake kuendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo ya Wananchi wa Tanzania mara baada ya utiaji saini Mkataba wa ujenzi wa jengo la Upasuaji Hospitali ya Micheweni Pemba.  
Picha Hassan Issa –OMPR–ZNZ.                                 

 Press Release:-


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kutoa ajira maalum kwa Watendaji wa Sekta ya Afya watakaotoa huduma  za afya Kisiwani Pemba ili kujaribu kuondosha tatizo la uhaba wa watendaji wa sekta hiyo.
Alisema mpango huo utakuwa wazi  na kutangazwa kwa watendaji wenye sifa za kufanya kazi hiyo  watakuwa huru kuomba nafasi hizo na yule atakayeamua kutumia fursa hiyo kwakufanya  ujanja wa kuchukuwa uhamisho kufanya kazi unguja  atambue mapema kwamba amejifukuzisha kazi mwenyewe.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo mara baada ya utiaji saini Mkataba wa uendelezaji wa Ujenzi wa Jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Micheweni uliofanywa kati ya Kaimu Balozi wa Japan Nchini Tanzania Bwana Kazuyoshi Matsunaga na Afisa Uendeshaji Tiba Kisiwani Pemba Bwana Ali Moh’d Mbarawa.
Mradi wa Ujenzi huo  uliobuniwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Jimbo la Konde ndani ya Wilaya ya Micheweni umepata mchango kutoka Serikali ya Japani kupitia Mradi wake wa kusaidia jamii wa GGHSP, Halmashauri ya Wilaya ya Micheweni, Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Mifuko ya Majimbo Manne ya Wilaya ya Micheweni .
Balozi Seif alisema ipo tabia ya muda mrefu  isiyoridhisha kwa watendaji wengi wa Sekta ya Afya kuomba ajira Kisiwani Pemba na Baadae kutumia mbinu na ujanja wa kusingizia ndoa pamoja na magonjwa  kuomba uhamisho wa kuhamia kufanya kazi Kisiwani Unguja.
Alisema tabia hiyo imeigharimu hasara kubwa Serikali Kuu pamoja na Wizara inayohusika na masuala ya Afya sambamba na kuleta usumbufu kwa wananchi wengi wanaohitaji huduma za Afya Kisiwani Pemba.
“ Hili kupitia kikao hichi nalisema wazi na kweupe kwamba tuitajipanga kutangaza nafasi za kazi kwa huduma za afya maalum kwa Pemba ili tutoe fursa kwa watendaji hao kusaidia ndugu na jamaa zao. Sasa kama kutakuwa na Mtu mjanja aelewe kwamba akifanya hivyo ajue kuwa kazi basi “. Alitahadharisha  balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kupeleka huduma zote muhimu kwa Wananchi wake katika maeneo yote ya Visiwa vya Unguja na Pemba bila ya kupendelea upande mmoja.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jumuiya ya Maendeleo ya Jimbo la Konde Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wa umakini wake wa kubuni mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo la Upasuaji katika Hospitali ya Micheweni.
Alisema ujenzi wa jengo hilo unaoendelea tokea Oktoba mwaka 2012 umekuja kwa wakati na ni muhimu kwa ustawi wa afya za wananchi wa Wilaya ya micheweni.
Alisema Mradi huo kwa kiasi kikubwa utasaidia kuwapunguzia akina mama shida ya kufuata huduma ya upasuaji wanapokuwa wajawazito katika hospitali za Wilaya nyengine.
“ Wenzetu hawa akina mama wajawazito wanapohitaji huduma ya upasuaji ni lazima kuwapatia haraka vyenginevyo tunahatarisha  maisha yao kwani bado suala la kupunguza idadi ya vifo vya wajawazito na watoto wachanga ni changamoto “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba jitihada mbali mbali zinazochukiliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kustawisha afya za wananchi wake imelenga kuondosha kabisa vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga.
Akitoa Taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la Upasuaji la Hospitali ya Micheweni Katibu wa Jumuiya ya Maendeleo ya Jimbo la Konde Nd. Ismail Juma alisema ujenzi wa Mradi huo ulioanza Mwezi Oktoba mwaka 2012 umekuja kufuatia shida za huduma za afya walizokuwa wakizipata Wananchi wa Wilaya ya Micheweni.
Nd. Ismail alisema wananchi wengi wanaokadiriwa kufikia wagonjwa 20 kwa mwezi hasa akina mama na watoto walikuwa wakilazimika kufuata huduma hizo katika Hospitali za Wete, Chake chake na Abdulla Mzee Mkoani.
Alisema mradi huo wa ujenzi wa jengo la upasuaji katika Hospitali ya Micheweni unatarajiwa kuhudumia wakaazi wapatao Laki 103,856 wa Majimbo Mnne yaliyomo ndani ya Wilaya ya Micheweni unakadiriwa kugharimu shilingi za Kitanzania Milioni 340,000,000/-.
Mapema Kaimu Balozi wa Japani Nchini Tanzania Bwana Kazuyoshi Matsunaga alisema Hospitali za Wilaya kwa mujibu wa vigezo vya vya Kimataifa zinalazimika kuwa na uwezo wa kutoa huduma muhimu za afya ukiwemo upasuaji.
Kaimu Balozi Katsunaga aliwahakikishia Wananchi wa Micheweni kwamba Serikali ya Japani kupitia mradi wake iliyouanzisha mwaka 1991 wa kusaidia huduma za Kijamii Nchini Tanzania katika sekta za Afya, Elimu na Maji kwamba mradi huo utakamilika kwa wakati ulipangwa.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Nchi yake itaendelea kutoa msaada pamoja na kuunga mkono miradi iliyoanzishwa na wananchi wa Tanzania na Zanzibar kwa ujumla katika lengo la kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa Kidiplomasia kati ya pande hizo mbili rafiki.