Afisa mdhanini Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Nd. Said Iddi
Hamad wa pili kutoka kulia akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif aliyepo Kushoto kuhusu uamuzi wa Wizara hiyo wa kuwapimia Viwanja Wananchi
katika eneo la Kifoi Wete ambalo limeleta mzozo na Kamisheni ya Wakfu Kisiwani
Pemba. Picha na Hassan Issa –
OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akikata Sabuni ya Mchi kuangalia ubora wake wakati
alipoutembelea ushirika wa akina Mama wa kutengeneza sabuni za Miti na za
kukogea wa Miti Ulaya Wete Kisiwani Pemba akishuhudia wa wanaushirika huo kulia
yake. Nyuma ya
Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mheshimiwa Omar Khamis Othman. Picha na Hassan Issa –
OMPR – ZNZ
Mshika fedha wa Ushirika wa akina mama wa kutengeneza sabuni za Miti na za
kukogea wa Miti Ulaya Wete Kisiwani Pemba Bibi Maryam Rashid Moh’d akimuonyesha
Balozi Seif Kidumu cha Sabuni za Kuogea wanazozalisha kwenye kiwanda chao. Wa mwanzo
kushoto ni Mwanachama wa Ushirika huo wa Selem Women Center Miti Ulaya Wete
Bibi Naima Abdulla. Picha na Hassan Issa –
OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuonya Uongozi wa Kamisheni ya
Wakfu na Mali Amana Kisiwani Pemba kusitisha mara moja zoezi la uwekaji wa Mabango
ya kuzuia ujenzi wa Nyumba katika eneo
la ardhi lenye mzozo liliopo Kifoi – Limbani Wete pamoja na lile la Junguni Gando
Kisiwani Pemba.
Amesema
iwapo Uongozi huo wa Wakfu na Mali ya Amana ulikuwa ukitekeleza agizo uliyopewa
na Kiongozi yeyote yule suala hilo litajadiliwa katika Vikao vya Baraza la
Mapinduzi Zanzibar hapo baadaye.
Balozi Seif
Ali Iddi alitoa onyo hilo alip[ofanya ziara fupi kukagua eneo hilo ambalo
limekuwa na mgogoro wa muda mrefu kati ya Kamisheni ya Wakfu na wananchi
waliopewa viwanja na mamlaka husika kujenga nyumba za kuishi.
Alisema eneo
hilo la Kifoi Limbani Wete Pemba ni miongoni mwa Maeneo ambayo Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar iliyagawa kwa Wananchi eka tatu tatu mara tu baada ya
Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ili waendeleze shughuli za Kilimo.
Alifahamisha
kwamba Hati zote zilizotolewa na kutumika kuhusu umiliki wa matumizi ya Ardhi
katika Visiwa vya Zanzibar kabla ya mwaka 1964 hazitumiki tena na kwa sasa ni
batili.
Balozi Seif
alisisitiza kwamba ardhi yote ya Visiwa vya Zanzibar ni mali ya Serikali. Hivyo
alisema mipango yoyote itakayoamuliwa na Serikali katika matumizi ya ardhi hiyo
popote pale ndani ya Zanzibar ni lazima iheshimiwe na Wananchi pamoja na
Taasisi ziwe za umma na hata binafsi.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alikemea kwamba kitendo cha Uongozi wa Kamisheni ya
Wakfu na Mali Amana Pemba kuendesha zoezi la uwekaji wa Mabango ya kuzuia
ujenzi linaweza kuamsha chuki, uhasama na hatimae kusababisha vurugu za kuvunja
amani.
“ Naagiza
kwamba zoezi la Wakfu na Mali ya Amana lisimame mara moja na mabango yote
yaliyowekwa yang’olewe. Nikimaliza vikao vya Baraza la Wawakilishi Unguja
vinavyoendelea hivi sasa nitafanya ziara ya kuja kungalia kama agizo langu
limetekelezwa “. Alisisitiza Balozi Seif.
Aliuasa Uongozi
huo wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Pemba kwamba hauna idhini ya kuzuia
Mashamba yaliyogawa Serikali eka tatu tatu kwa Wananchi mwaka 1964 bali wanachokifanya
ni uamuzi wa Watu binafsi na kamwe hilo ni jambo lisilokubalika.
Akitoa
ufafanuzi Afisa Mdhamini Wizara ya
Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Pemba Ndugu Said Iddi Hamad alimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wizara hiyo kupitia Idara ya Ardhi na Mipango
Miji ilikata viwanja na kugaia Wananchi kwa lengo la kujenga nyumba za Kuishi.
Nd. Said
alisema hatua hiyo imekuja baada ya eneo hilo kuanza kuvamiwa na kuanzishwa
ujenzi holela jambo ambalo Taasisi ya Ardhi
ikalazimika kuchukuwa hatua za kitaalamu za kulipima eneo hilo katika
mfumo unazingatia mipango miji.
Mapema Sheha
wa Shehia ya Limbani Bwana Masoud Ali Hassan alisema kwamba eneo hilo la Kifoi
– Limbani Wete limegaiwa kwa Wananchi Eka Tatu tatu maara baada ya Mapinduzi ya
Zanzibar ya mwaka 19664.
Sheha Masoud
alisema shughuli za ujenzi wa makaazi ya
nyumba za kudumu ndani ya eneo hilo ulianza zaidi ya miaka 20 baada ya
Mapinduzi kukiwa hakuna malalamiko wala
madai dhidi ya wahusika hao.
Alisema
anashangaa kuona Uongozi wa Kamisheni ya Wakfu na Mali ya Amana Kisiwani humo
ukiendesha zoezi la uwekaji wa mabango ya kuzuia ujenzi au shughuli zozote
katika kipindi hichi ukidai kwamba hiyo ni shmba na Wakfu ya Marehemu Bwana
Abdullah Bin Suleiman El – Busaid wa Limbani Wete.
Naye Mkuu wa
Mkoa wa Kaskazini Pemba Mh. Omar Khamis Othman alieleza masikitiko yake dhidi
ya Uongozi wa Taasisi hiyo ya Wakfu Pemba kwa kuchukuwa hatua za uendeshaji wa
zoezi hilo bila ya kuiarifu Serikali ya Wilaya ya Wete wala ile ya Mkoa wa
Kaskazini Pemba.
Mh. Omar
alisema Uongozi huo ulichukuwa uamuzi huo bila ya kuzingatia kwamba maeneo
wanayoyapima hivi sasa yanatumiwa na wananchi kwa kazi na shughuli mbali mbali
za kilimo pamoja na ujenzi.
Wakati huo
huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikitembelea
kikundi cha Ushirika wa Akina Mama cha Utengenezaji wa Sabuni za Michi na kukogea
cha Miti Ulaya Mjini Wete.
Akizungumza
na wana ushirika hao Balozi Seif aliwataka akina mama hao kuendelea
kuzingatia vyema maadili na taratibu
zilizowekwa kuhusu uendeshaji wa vikundi vya ushirika.
Alisema vipo
vikundi vingi vilivyoanzishwa hapa nchini na kuanza vyema shughuli zao za
uzalishaji lakini vikashindwa kudumu kutokana na baadhi ya wanachama wake hasa
wale viongozi waliopewa dhamana kukosa maadili.
Akizungumzia
suala la uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi oktoba mwaka huu Mkamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wana ushirika hao ni vyema
wakawalinganisha mapema viongozi wenye nia safi ya kukubali kuwatumikia.
“Baadhi ya
waheshimiwa wamekuwa na tabia zinazofanana na simu ya mkononi. Wakeshaichaji hawana habari tena na wale
waliowachagua. Hivi sasa wameanza kutafuta waya wa kuchajia kwa sababu uchaguzi
umekaribia “. Balozi Seif aliwatahadharisha akina mama hao.
Balozi Seif
aliupongeza Uongozi na wana ushirika wa Utengenezaji wa Sabuni za Michi na
kukogea Miti Ulaya Wete kwa uwekaji wa kumbu kumbu za matumizi na kuahidi
kuwalipia deni lao wanalodaiwa katika shughuli za ujenzi wa Jengo lao la
kudumu.
Mapema Mke
wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi aliwataka akina
mama hao kujituma zaidi katika miradi yao ya kuiuchumi na maendeleo kwani wao
ndio walezi wakuu wa familia.
Mama Asha
alisema hayo hayata patikana wala kufanikiwa iwapo akina mama hao kwa
kushirikiana pamoja na akina bab hawatadumisha Umoja, Mshikamano na upendo
miongoni mwao.
Mke huyo wa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika kuunga mkono juhudi za akina Mama hao
wa Kiwanda cha utengenezaji wa Sabuni za michi na kuogea aliahidi kukichangia
shilingi Milioni 3,000,000/- ili zisaidie kupunguza changamoto zinazowakabili
ikiwemo baadhi ya vifaa na mali ghafi za mradi wao.