Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akikagua maendeleo ya
ujenzi wa Skuli ya Jamii katika Kijiji cha Kiwengwa Mkoa wa Kaskazini Unguja. Kushoto ya
Balozi Seif ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo Bwana Tahir Ali,
Kulia yake Balozi Seif ni Mkewe Mama
Asha Suleiman Iddi ambapo nyuma yao ni jengo la Vyoo lililojengwa kwa kutumia
chupa za maji zilizotiwa mchanga. Picha na
Hassan Issa–OMPR
Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kulia akimpongeza Meneja wa Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Nchini Marekani Bwana Josh Winter kutokana na Taasisi yake kusaidia maendeleo ya Elimu Zanzibar. Picha na Hassan Issa–OMPR
Press Release
Maendeleo ya
ujenzi wa Skuli ya Msingi ya Jamii katika kijiji cha Kiwengwa Kiliomo ndani ya
Wilaya ya Kaskazini “ B “ yanaendelea vyema katika hatua za mwisho zitakazoiwezesha
skuli hiyo kuanza kuchukuwa wanafunzi wa Elimu ya maandalizi kuanzia mwezi
Januari Mwaka ujao wa 2016.
Ujenzi wa
skuli hiyo uliohusisha pia vyoo na Tangi la Kuhifadhia maji ambavyo vinajengwa
kwa kutumia Taaluma ya Chupa za Maji
zilizotiwa mchanga unafadhiliwa na Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka
Nchini Marekani.
Makundi ya
Wanafunzi wa Vyuo na Skuli mbali mbali za Sekondari Kutoka Nchini Marekani kwa
kushirikiana na Wanakijiji wa Kiwengwa
wamekuwa wakipiga kambi wakiendelea na kazi mbali mbali za kujitolea katika
ujenzi huo wa aina yake.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Ujenzi wa Skuli hiyo Bwana Tahir Ali alimueleza Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyepeta fursa ya kukagua maendeleo ya
ujenzi huo kwamba Kamati hiyo kwa kushirikiana na Wananchi kupitia ushauri wa
Wizara husika ya Elimu wanatarajia kuanza usomeshaji mapema mwakani kwa hatua
ya watoto wa maandalizi.
Bwana Tahir
alisema juhudi za Wanakijiji kwa kuungwa Mkono na Shirika la Kimataifa la Give
la Marekani zimelenga kuwakomboa Watoto wa Kijiji hicho ambao kwa muda mrefvu
walikuwa wakikosa fursa muhimu za kielimu.
Naye Meneja
Mpya wa Mradi wa Kimataifa wa Give kutoka Marekani Bwana Joshi Winter alisema Uongozi
wa Mradi huo umejipanga vyema katika kuhakikisha ujenzi wa Skuli hiyo
unakamilika vizuri na kutoa fursa kwa watoto wa Kijiji hicho kupata Elimu.
Bwana Josh
alisema hatua zimeandaliwa vizuri katika kuyapatia madeshi madarasa ya skuli
hiyo, Huduma za Maktaba sambamba na Kompyuta zitakazowawezesha wanafunzi
watakaoingia katika skuli hiyo wanapata taaluma yenye mfumo wa kisasa wa mawasiliano ya Sayansi na
Teknolojia.
Meneja wa
Mradi huo wa Give ameuomba Uongozi wa Kijiji hicho kwa kushirikiana na Serikali
Kuu kuandaa mazingira ya kupata eneo kubwa zaidi kwa ajili ya matayarisho ya
ujenzi wa Majengo ya Sekondari katika Skuli hiyo ya Jamii Kiwengwa ambapo
Taasisi yake itakuwa tayari kusaidia ufadhili.
Akitoa
shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Taasisi
hiyo ya Kimataifa inafaa kupongezwa na wapenda Elimu hapa Nchini kutokana na
hatua yake ya kuunga mkono makundi ya jamii katika kujikomboa kielimu.
Balozi Seif
alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini juhudi za taasisi na
mashirika ya maendeleo ndani na nje ya nchi yaliyojitolea kusaidia Wananchi
hasa wanaoishi katika mazingira magumu ya kimaisha ambayo huwa kikwazo cha
kupata elimu.
Akizungumza
na Wanafunzi wa Kujitolea kutoka Vyuo na Skuli mbali mbali za Marekani
alipotembelea maendeleo ya ujenzi huo Mwezi Mei mwaka uliopita Balozi Seif
aliwapongeza wanafunzi hao kwa uamuzi wao wa kusaidia Maendeleo ya Elimu katika
Visiwa vya Zanzibar.
Taaluma ya matumizi ya chupa za Maji
zinazotiwa mchanga iliyobuniwa Nchini Nicaragua Amerika Ya Kusini katika ujenzi
wa majengo mbali mbali ya makazi na huduma za Kijamii inatumika kwa lengo la
kutunza mazingira.