Mwalimu wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar
{Special Olympic} Maalim Amour Ali
Khamis akisoma risala wakati wa hafla
fupi ya kukabidhi medali za ushindi kwa
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenye mashindano ya
Kitaifa yaliyofanyika Kibaha. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Michezo cha Watu wenye ulemavu wa
Akili Zanzibar Bibi Saada Hamad Ali akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Balozi Seif Medali 32 walizopata wachezaji wa Zanzibar katika
mashindano ya Kitaifa Mkoani Kibaha. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Balozi Seif akimvisha Medali Mchezaji Fahad Juma Khamis ambae
alishinda kwenye mashindano ya Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Pwani Tanzania
Bara. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Mchezaji Huzaima Haji Ali wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa Akili
Zanzibar akivishwa Medali na Balozi Seif baada ya kushinda mashindano ya Kibaha
Tanzania Bara. Picha na Hassan Issa –
OMPR
Baadhi ya wachezaji wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa
Akili Zanzibar wakifuatilia hotuba ya Balozi Seif ambaye hayupo pichani wakati
akiwapongeza baada ya kufanya vizuri kwenye mashindano yao. Wa kwanza
kutoka kulia ni mchezaji wa soka Mbarak Awesu Moh’d wa Zanzibar aliyebahatika
kuwa miongoni mwa Wachezaji wa Tanzania watakaokwenda Nchini Marekani kushiriki
mashindano ya Kimataifa.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Picha na Hassan Issa – OMPR
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Timu ya Mchezo wa
Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar baada ya kuwapongeza kwa kuja na ushindi
Zanzibar.
Picha na Hassan Issa – OMPR
Picha na Hassan Issa – OMPR
Press Release
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Chama cha
Michezo cha Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar {Special Olympic} kwa jitihada uliochukuwa kwa kuiwezesha Timu
ya Zanzibar kurejea na ushindi mkubwa kwenye mashindano ya Taifa yaliyofanyika
Kibaha Tanzania.
Alisema jina
la Zanzibar tayari linaanza kuibika tena kwenye medani ya Michezo katika Nyanja
ya Kimataifa baada ya kufifia katika miaka ya nyuma kutokana na kukosa kutoa
wachezaji wenye kiwango kinachokubalika Kimataifa.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa Pongezi hizo Ofisini
kwake Vuga Mjini Zanzibar baada ya kupokea Medani 32 ambazo kati ya hizo 17 za dhahabu, Tano za
Fedha na 10 za Shaba walizopata wachezaji wa Zanzibar kwenye mashindano hayo.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar amefarajika kutokana na ushindi huo na kushawishika
kuwavisha nishani hizo baadhi ya wachezaji hao akiwemo Mbarak Awesu Moh’d
aliyefanikiwa kuchaguliwa katika Timu ya Taifa ya Tanzania inayotarajiwa
kushiriki mashindano ya Kimataifa ya Special Olympic Nchini Marekani Mwezi uajo
wa Julai mwaka huu.
Balozi Seif
alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ilani ya Chama cha mwaka 2010
iliyotilia Mkazo Michezo itajitahidi kutoa msukumo katika kuunga mkono michezo
hasaya wachezaji vijana wenye mahitaji maalum.
Katika
kuunga mkono jitihada za Viongozi na wachezaji hao wa Special Olympic Balozi Seif alitoa ahadi
kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itagharamia Tiketi kwa Mchezaji Mbarak
Awesu Moh’d wa Zanzibar aliyebahatika kuwa miongoni mwa Wachezaji wa Tanzania
watakaokwenda Nchini Marekani.
Akisoma
Risala ya wanamichezo hao Mwalimu wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu wa
Akili Zanzibar {Special Olympic} Maalim
Amour Ali Khamis alisema chama cha
Mchezo huo kimesajiliwa Tarehe 12 Oktoba mwaka 2009 kwa lengo la kuendeleza
michezo kwa watu wenye akili pungufu.
Maalim Amour
alisema ufinyu wa fedha unaokikabili chama cha mchezo huo Zanzibar umechangia
kukosa ushiriki sahihi wa wachezaji wa mchezo huo kwa pande zote mbili za Zanzibar katika
mashindano ya Kitaifa.
Mwalimu huyo wa Timu ya Mchezo wa Watu wenye ulemavu
wa Akili Zanzibar {Special Olympic} kwa niaba ya Viongozi na wachezaji
waliochini ya Chama hicho ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa
uamuzi wake wa kuunga Mkono timu yao.
Alisema
jitihada hizo za Serikali kwa kushirikiana na wafadhili tofauti kutoka Taasisi
za Umma na Watu Binafsi zimewawezesha
Vijana hao wa Zanzibar kushiriki michezo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Akimkabidhi
Medali hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Makamu
Mwenyekiti wa Chama cha Michezo cha Watu wenye ulemavu wa Akili Zanzibar Bibi
Saada Hamad Ali alisema vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa watoto wenye
ulemavu wa akili hivi sasa vimekithiri mno.
Bibi Saada
alisema inasikitisha kuona baadhi ya wasimamizi wa sheria wanakataa ushahidi
unaotolewa na wazazi au walezi wa watoto wenye ulemavu wa akili kwa kisingizio
kwamba ushahidi kamili haujakamilika.
Alisema
jamii inaendelea kushuhudia udhalilishaji huo kwa kuwapa nguvu watu waovu kuendeleza
vitendo viovu kutokana na kuelewa kuwa wanaotendewa vitendo hivyo kati yao
wanashindwa kujieleza mahakamani kutokana na ulemavu wao.