Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akisalimiana na Vijana na wazee wa Fujoni Nyumba ya Ndege alipokwenda
kutekeleza ahadi yake ya kusaidia ujenzi wa uwanja wa michezo wa Fujoni
Boys { Hibury }. Picha Hassan Issa –
OMPR – ZNZ.
Balozi Seif akimkabidhi fedha Taslim Shilingi Milioni 4,000,000/- Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “ Nd. Hilika Ibrahim kwa ajili ya matengenezo ya uwanja wa michezo wa Timu ya Soka ya Fujoni Boys. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Balozi Seif akimkabidhi fedha Taslim Shilingi Milioni 4,000,000/- Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “ Nd. Hilika Ibrahim kwa ajili ya matengenezo ya uwanja wa michezo wa Timu ya Soka ya Fujoni Boys. Picha Hassan Issa – OMPR – ZNZ.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi
akiwapongeza wananchi wa Fujoni kwa umakini wao wa kutetea na kulinda sera za
Chama Tawala kinachoonbgoza Dola Tanzania. Picha Hassan Issa –
OMPR – ZNZ.
Press Release:-
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balizi Seif Ali Iddi amewaasa Wazee Nchini kuwadhibiti
watoto wao kutojiingiza katika makundi yanayoandaliwa na baadhi ya watu
wakiwemo wanasiasa kufanya vurugu zinazoashirika kutaka kuvuruga amani ya Nchi.
Akaonya
kwamba asijetokea mzazi atakayetaka kuilaumu Serikali wakati vyombo vyake vya
dola vitakavyotekeleza majukumu yake
katika kuwadhibiti watu watakaobainika kusababisha vurugu ndani ya kipindi hichi
kinachoelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba.
Balozi Seif
Ali Iddi ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la
Kitope alitoa wosia huo wakati akikabidhi mchango wa shilingi Milioni
4,000,000/- akitekeleza ahadi aliyotoa
tarehe 4 June mwaka huu kusaidia matengenezo ya uwanja wa michezo wa
Timu ya soka ya Fujoni Boys { HIBURY } hafla iliyofanyika katika Maskani ya Nia
Njema Nyumba ya Ndege Fujoni.
Balozi Seif alisema
Serikali ina taarifa kwamba wapo watu na baadhi ya wanasiasa waliojiandaa
kifedha kuwashawishi vijana kujiingiza katika makundi na kufanya vurugu ndani
ya zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya kupiga kura pamoja na uchaguzi wa
mwezi Oktoba.
Aliwatahadharisha
Wazazi pamoja na Vijana kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya Dola iko makini
na tayari imeshajiandaa kukabiliana na vurugu ama njama yoyote itakayoandaliwa
ya kutaka kujaribu kutia doa zoezi hilo la uandikishaji wapiga kura pamoja na
uchaguzi Mkuu.
Alifahamisha
kwamba inasikitisha kuona mtego huo unaoandaliwa na kuwahusisha zaidi Vijana mara
zote unafanywa na watu wanaokuwa mbali na matatizo yanayowakumba vijana hao
baada ya kuhusika na vurugu hizo.
“ Wazee
lazima wajizatiti katika kuhakikisha wanawanusuru watoto wao na mtego
unaoandaliwa na watu wenye nia na muelekeo wa maslahi yao binafsi “. Alisema
Balozi Seif.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba wapo Watu na baadhi ya makundi
yasiyoitakia kheir nchi hii ambao tayari wameshaanza kuonyesha dalili za
kuleta Vurugu.
Balozi Seif
aliwahakikishia Wananchi wote Nchini kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
na Ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zitajitahidi kuona amani na utulivu
wa Nchi unaendelea kudumu katika muda wote.
Akigusia
kitendo cha Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Chama cha Wananchi { CUF }
kutoka kwenye Kikao cha Baraza la Wawakilishi kilichokuwa kikiendelea kwenye
Baraza hilo Mbweni hapo juzi Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar alisema uamuzi wao haukuzingatia upeo wa Demokrasia ya
mfumo wa vyama vingi wa Siasa uliopo hapa Nchini.
Balozi Seif
akiwa Mtendaji Mkuu wa Serikali alielezea masikitiko yake kutokana na uwamuzi
wa Wajumbe hao wa Upande wa Upinzani uliokuwa na nia ya kutaka kuvuruga mfumo
mzima wa muenendo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar unaofuata Mfumo wa Umoja
wa Kitaifa.
Alisema ususiaji
wa Wajumbe hao katika Vikao vya Baraza hilo lililokuwa likijadili na kutaka
kupitisha matumizi ya Serikali yalikuwa na lengo la kutaka kuzuia matumizi
halisi ya fedha kwa Taasisi za Umma za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jambo
ambalo lingevuruga mfumo mzima wa uendeshaji wa Serikali.
“ Licha ya
misaada ya baadhi ya wahisani lakini fedha nyingi zinazotumika kwenye uchaguzi
wetu zinatoka katika mfuko Mkuu wa Serikali. Sasa mbinu za Wajumbe hao kukimbia
kupitisha makadirio ya matumizi kwa Wizara inayosimamia fedha zinaashiria
kutaka kuharibika kwa uchaguzi Mkuu “. Alifafanua Balozi Seif.
Mapema Mke
wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema Viongozi
na wanachama wa vyama vya Upinzani ni vyema wakazingatia umuhimu wa kuwa na uvumilivu
wa kisiasa ndani ya mfumo wa vyama vingi
vya siasa hapa Nchini.
Mama Asha
alisema yapo mambo na baadhi ya matukio yenye kuleta kero na hata usumbufu kwa
Viongozi na Wanachama wa Chama cha Tawala cha CCM lakini wana CCM hao wanalazimika kukubali kuvumilia
kwa lengo la kudumisha amani na upendo miongoni mwa jamii.
Amewapongeza
Wananchi wa Fujoni kwa msimamo wao madhubuti wa kulinda na kutetea sera za
Chama Tawala cha Mapinduzi zilizopata ridhaa za wananchi walio wengi kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 na kupata fursa
ya kuongoza Dola.