Monday, 8 June 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitembele Mradi wa Ujenzi wa Bara bara inayoanzia Kiashangwe Mkwajuni hadi Mbuyu Tende Matemwe

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akitembele Mradi wa Ujenzi wa Bara bara inayoanzia Kiashangwe Mkwajuni hadi Mbuyu Tende Matemwe unaotekelezwa na Kampuni ya Penny Royal inayosimamia mradi mkubwa wa ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa itayopewa jina Zanzibar Amber Resort. Kulia ya Balozi Seif ni Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Zanzibar Amber Resort kwa upande wa Zanzibar Bibi Naila Jidawi.  Picha na Hassan Issa -OMPR
Balozi Seif akielezea faraja yake mbele ya Uongozi wa Zanzibar Amber Resort kutokana na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa barabara hiyo itakayosaidia kuondosha usumbufu wa mawasiliano Wananchi wa Maeneo ya Matemwe Mbuyu Tende. Kulia ya Balozi ni Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Zanzibar Amber Resort huko Matemwe unaosimamiwa na Kampuni ya Penny Royal Bwana Brian na Msimamizi wa Mradi huo kwa upande wa Zanzibar Bibi Naila Jidawi. Picha na Hassan Issa-OMPR
Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Zanzibar Amber Resort huko Matemwe unaosimamiwa na Kampuni ya Penny Royal Bwana Brian kati kati akimuonyesha Balozi Seif ramani halisi itakavyokuwa ya ujenzi wa Hoteli hiyo. Mwanzo kutoka kulia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja Nd.Haji Juma haji na mwanzo kulia ni msimamizi wa Mradi huo kwa upande wa Zanzibar Bibi Naila Jidawi. Balozi Seif akiwanasihi Wananchi wa Kijiji cha Matemwe kuendelea kushirikiana na muwekezaji aliyejitokeza kuweka mradi mkubwa wa Kiuchumi wa Hoteli ya Zanzibar Amber Resort ndani ya Kijiji chao. Picha na Hassan Issa -OMPR


















Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimpongeza Msimamizi wa Mradi wa Hoteli wa Zanzibar Amber Resort kwa upande wa Zanzibar Bibi Naila Jidawi kwa jitihada zake zilizofanikisha kuanza kutekelezwa kwa mradi huo. Picha na Hassan Issa-OMPR

Press Release
Wananchi wa Kijiji cha Matemwe wameshauriwa kuendelea kushirikiana naWawekezaji walioamua kuwekeza miradi yao ndani ya maeneo yao baada ya kupata ridhaa ya Serikali ili miradi inayoanzishwa iweze kuwasaidia kimapato na kukidhi mahitaji yao ya kimaisha ya kila siku. 
Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Bara bara ya Kilomita 12 yenye kujengwa na Kampuni ya Penny Royal inayotaka kuanzisha mradi mkubwa wa Hoteli ya Kimataifa itakayopewa jina la Zanzibar Amber Resort katika kijiji cha Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Balozi Seif alisema Wananchi wa Kijiji cha Matemwe wanapaswa kuendelea kuwa tofauti na Wananchi wa maeneo mengine nchini kufuatia bahati waliyoipata ya kuanzishwa kwa mradi mkubwa wa kiuchumi ndani ya kijiji chao jambo ambalo baadhi ya wenzao huonyesha kuhitilafiana na Wawekezaji wanaojitokeza. 
Alisema kazi iliyo mbele yao Wananchi hao hasa Vijana ni kujituma zaidi katika kutafuta Elimu itakayokuja wapa fursa za kupata ajira katika mradi huo Mkubwa unaotarajiwa kutoa nafasi za ajira zisizopungua Elfu 1,000.
Balozi Seif alifahamisha kwamba zipo kazi mbali mbali zitakazoibuka ndani ya mradi huo wa Zanzibar Amber Resort ambazo zinahitaji kuchangamkiwa na Wananchi Wazalendo badala ya kulemaa na hatimae kujachukuliuwa na Wafanyakazi wa Kigeni.
 “ Wananchi msipokuwa makini hasa vijana katika kujiandaa kusaka elimu kwa ajili ya nafasi hizo itafikia wakati wa kuanza kusikitika na kuilalamikia Serikali kwa kukosa fursa za kazi “. Alisema Balozi Seif. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na wawekezaji wowote waliokubali kuwekeza miradi yao ya Kiuchumi hapa Nchini.
Alisema katika kuunga mkono juhudi za wawekezaji hao Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imeshaupitisha mradi huo wa Zanzibar Amber Resort baada ya kukamilisha taratibu zinazohitajika katika masuala ya uwekezaji.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Zanzibar Amber Resort huko Matemwe unaosimamiwa na Kampuni ya Penny Royal Bwana Brian Thomson alisema Uongozi wa Mradi huo umemua kuanza na ujenzi wa Barabara ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wa eneo hilo pamoja na watendaji wa mradi huo wakati ujenzi utakapoanza rasmi.
Bwana Brian alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi huo utakwenda sambamba na ujenzi wa Skuli, Hospitali, Kituo cha Polisi sambamba na ujenzi wa Kituo cha Jamii kitakachowapa fursa Wananchi wa Matemwe hasa wajasiri amali kuendesha miradi yao katika eneo la kisasa.
Alifahamisha kwamba Uongozi wa Zanzibar Amber Resort umekusudia kufanyakazi kwa karibu zaidi na Jamii mpango utakaosaidia kuleta mafanikio makubwa kati ya pande hizo mbili pamoja na Serikali Kuu. Mendaji Mkuu huyo wa Mradi wa Zanzibar Amber Resort alieleza kwamba mradi huo pia utajenga uwanja wa ndege na kiwanja cha mchezo maarufu wa Golf ambao hupendwa zaidi na matajiri wakubwa katika maeneo mbali mbali Ulimwenguni.
“ Mradi wetu mkubwa utakaokuwa na kiwanja cha ndege na mchezo maarufu unaopendwa na matajiri wengi Duniani wa Golf tunamategeo ya kuzalisha ajira nyingi zitakazowapa fursa wananchi wazalendo kupata ajira za kujiendesha kimaisha “. Alifafanua Bwana Brian.
Akitoa ufafanuzi Msimamizi Mkuu wa Mradi wa Zanzibar Amber Resort kwa upande wa Zanzibar Bibi Naila Jidawi alisema kwamba Wataalamu wa Kampuni inayosimamia mradi huo watatengeneza Visiwa vidogo vidogo kwa kufukia Bahari ili kuongeza mandhari nzuri ya mradi huo wa Hoteli. Bibi Naila alisema miradi ya kufukia Bahari ambayo hufanyika katika baadhi ya Nch Duniani huzingatia utaalamu mkubwa wa hali ya juu chuni ya usimamizi wa wataalamu wa Bahari, hali ya hewa pamoja na wale wa mazingira.
Alisisitiza kwamba matengenezo hayo ya visiwa vidogo vidogo yatakwenda sambamba na ujenzi wa mkahawa maalum utakaojengwa chini ya Bahari zikiwemo nyumba za wafanyakazi. Huu ni mradi wa pili wa ujenzi wa majengo yanayotoa huduma za wageni na watalii ndani ya Bahari katika Visiwa vya Zanzibar ukitanguliwa na ule wa Chumba cha chini ya Bahari kilichojengwa katika Kijiji cha Makangale Mkoa wa Kaskazini Pemba karibu miaka mitatu iliyopita.