Tuesday, 9 June 2015

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akisema wakati umewadia kwa wanamichezo Nchini kufanyakazi kisayansi ili kuodoa mapungufu yanayopatikana katika sekta hiyo na kuirejeshea Heshima yake Tanzania katika Nyanja ya michezo Kimataifa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akisalimiana na Mwanariadha mkongwe wa Kimataifa wa Zanzibar  Suleiman Ame { Nyambui  } mara alipowasili katika Kijiji cha Filbert Bayi kufunga mashindano ya 54 ya Taifa ya Riadha Zanzibar.
Kushoto ya Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarest Lihilo.

Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania pamoja na washindi wa mbio za Mita 1,500 alizozishuhudia mwishoni mwa fainali za mashindano ya Riadha Taifa. Picha na Hassan Issa - OMPR – ZNZ.
Washindi wa mbio za Mita 1,500 kwenye mashindano ya riadha Taifa wakati ni mshindai wa kwanza wa mbio za Mita 1,500 Gabriel Gerald wa Mkoa wa Arusha, Kushoto yake mshindi wa pili Agostino Sudi wa Mkoa wa Arusha na kulia yake Silvester Simon wa Mkoa wa Kilimanjaro. Picha na Hassan Issa - OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kati kati waliosimama akiwa katika picha ya pamoja na Mabingwa wa Mashindano ya 54 ya Taifa Riadha Tanzania Mkoa wa Mjini Magharibi mara baada ya kuyafunga mashindano hayo Mkoani Pwani. Picha na Hassan Issa - OMPR – ZNZ.
Balozi Seif kati kati na Naibu Waziri wa Michezo Juma Ngamia wakiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa Mkoa wa Mwanza mara baada ya kuyafunga mashindano hayo Mkoani Pwani. Picha na Hassan Issa - OMPR – ZNZ.
Balozi Seif na viongozi wengine wa shirikisho la Riadha Tanzania akiwa katika picha ya pamoja na wachezaji wa tmu ya riadha ya Mkoa wa Kusini Unguja alipoamua kupiga picha nao baada ya kuyafunga mashindano yao Mkoani Pwani. Picha na Hassan Issa - OMPR – ZNZ.






















Balozi Seif akiwa katikam picha ya pamoja na wanafunzi wa Skuli ya Filbert Bayi waliohusika katika kazi ya ugawaji wa zawadi kwa washindi wa mashindano ya riadha Taifa Mkoani Kibaha. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Kijiji cha Filbert Bayi Bibi Anna Bayii na Naibu Waziri wa Michezo SMT Mh. Juma Ngamia. Picha na Hassan Issa - OMPR – ZNZ.

 Press Release:- 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umewadia kwa wanamichezo Nchini kufanyakazi kisayansi ili kuodoa mapungufu yanayopatikana katika sekta hiyo na kuirejeshea Heshima yake Tanzania katika Nyanja ya michezo Kimataifa.
Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imewahi kujiwekea rekodi nzuri ya ushindi Kimataifa hasa katika Mchezo wa Riadha ambapo ilipata nafasi ya kunyakua Medali mbali mbali kutokana na juhudi kubwa iliyokuwa ikifanywa na shirikisho la Riadha Nchini Tanzania.
Balozi Seif alieleza hayo wakati akiyafunga mashindano ya 54 ya Taifa ya mchezo wa Riadha yaliyokuwa yakifanyika kwa siku Tatu katika Shule ya Filbert Bayi Mkuza Kibaha Mkoani Pwani ambapo Mikoa 21 kati ya 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar ilishiriki kwenye mashindano hayo.
Alisema wanamichezo lazima wajiwekee malengo ya muda mfupi na mrefu wakati wanapohitaji mafanikio kwenye michezo yao na Serikali iko tayari kushirikiana kwa karibu na wanamichezo hao kwa nia ya kurejesha Heshima ya Tanzania iliyojengeka zamani.
Balozi Seif alifahamisha kwamba yapo mashindano mbali mbali ya Kimataifa ambayo Tanzania itawajibika kushiriki. Hivyo matayarisho ya mapema ni jambo la lazima katika hatma ya kufanikisha ushindi  kwenye mashindano hayo.
“ Tunayo mashindano ya Riadha ya Dunia yanayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu Nchini China, mashindano ya Afrika Mwezi Septemba mwaka huu Nchini Congo Brazaville ya yale ya Olympiki 2016 Reo De Janairo Brazil  ambapo tutalazimika kujizatiti ili kushiriki vyema na kurudi na ushindi “. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kuwa Taifa linatambua umuhimu wa Michezo na ndio maana Serikali zote mbili ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar ziliamuwa kuunda Wizara Maalum zinazosimamia na kushughulikia sekta ya Michezo.
Alifahamisha kwamba Michezo imeweza kuwaunganisha Watanzania kuwa kitu kimoja pamoja na kujenga ujirani mwema na urafiki kati yake na wenzao wa mataifa jirani.
Balozi Seif ambaye aliwahi kuwa mwanamichezo wakati wa enzi zake aliwanasihi washiriki walioshinda kwenye mashindano hayo ya kitaifa wasiridhike na ushindi walioupata na badala yake wajiwekee malengo ya kushinda katika michezo mengine ya Kimataifa watakayobahatika kushiriki.
Aliupongeza Uongozi Mzima wa Kijiji cha Michezo cha Filbert Bayi kwa kuwa na miundombinu bora ya kuibua vipaji wa wanamichezo nchini pamoja na Uongozi wa Shirikisho la Riadha Tanzania ambao umefanikisha mashindano hayo ikiwa ni uthibitisho tosha kuwa Shirikisho hilo liko hai na linatekeleza wajibu wake ipasavyo.
Akitoa Taarifa fupi ya mashindano hayo Msaidizi Katibu wa Shirikisho la Riadha Tanzania Bibi Ombeni Zavara alisema Mikoa yote 30 ya Tanzania Bara na Zanzibar ilipewa barua ya ushiriki wa mashindano hayo lakini  Mikoa iliyoshiriki  mashindano hayo ni   21.
Ombeni alisema michezo tofauti 16 ya wanaume na 13 ya wanawake imeshindaniwa kwenye mashindano hayo yaliyoanza mwaka 1964 baada ya kuasisiwa rasmi michezo ya riadha Tanzania mnamo mwaka 1961.
Msaidizi Katibu huyo wa Shirikisho la Riadha Tanzania aliuomba Uongozi wa Kila Mkoa  hapa Nchini kuhakikisha kwamba wanaendeleza michezo mbali mbali ili kupata fursa ya kuvilea vipaji vya vijana vinavyoibuka kwenye Mikoa hiyo.
Mapema Mkurugenzi wa Skuli ya Filbert Bayi Bibi Anna Bayi alisema Mkoa wa Pwani umeamua kutafuta vipaji vya wanamichezo wa pande zote mbili za Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaendeleza kwenye Kijiji cha vipaji cha Filbert Bayi.
Bibi Anna alisema juhudi hizo ni vyema zikaenda sambamba na uimarishaji wa miundo mbinu kwenye kijiji hicho kinachohitaji kuwa na uwanja unaokidhi kiwango kinachokubalika Kimataifa ambacho kitahitaji kuungwa mkono  kwa dhati na wadau wote wa michezo.
Alifahamisha kwamba Skuli hiyo ya Vipaji maaum imekusidia kwamba  mchezaji anayetoka kwenye kijiji hicho baada ya kupata taaluma akidhi vilivyo  kiwango kinachokubalika kuingia katika mashindano ya Kimataifa popote pale atakapoamua kwenda kushiriki.
Akitoa salamu za Shirikisho la Riadha Tanzania Makamu wa Rais wa Shirikisho hilo William Kalage alisema michezo ya Riadha inayosimamiwa na Taasisi yake inafuata Kalenda ya shirikisho la Riadha la Dunia Tanzania ikiwa mwanachama wake.
William Kalage alifahamisha kwamba katika kwenda sambamba na sheria na taratibu wa Shirikisho la Dunia la Mchezo wa Riadha Shirikisho la Riadha Tanzania tayari limeshapitisha Katiba iliyoridhiwa na kukubalika na Shirikisho hilo la Kimataifa.
Katika mashindano hayo ya 54 ya Riadha Taifa Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alibahatika kushuhudia fainali ya mbio za mita 1,500 ambapo mshindi wa kwanza alikuwa Gabriel Gerald wa Mkoa wa Arusha aliyetumia Dakika 3 Sekunde 53 na Nukta 3.
Mshindi wa Pili ni Agostino Sudi vile vile kutokea Mkoa wa Arusha aliyekimbia kwa Dakika 3 Sekunde 58 na Nukta 29 wakati mshindi wa Tatu alikuwa Silvester Simon kutoka Mkoa wa Kilimanjaro aliyetumia Dakika 3 Sekunde 28 na Nukta 28.
Matokeo ya jumla wanaume wa kwanza ni  Mkoa Mjini Magharibi akifuatiwa na Mkoa wa Pwani, Arusha, Dar es salaam, Kaskazini Unguja na Dodoma na Mara wakati Wanawake  washindi wa kwanza walikuwa Mjini Magharibi,Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Kaskazini Unguja, Pwani, Dar es salaam, Kusini na Kaskazini Pemba.
Ushindi wa jumla wa mashindano hayo ya riadha ya mwaka huu umechukuliwa na Mkoa wa Mjini Magharibi ulioibuka na Medali 27, wa Pili Mkoa wa Pwani, wa Tatu Mkoa Arusha na wa Nne ni Mkoa wa Dar es salaam.