Press release:-
Wazazi
wameaswa kuwa tayari kuwapokea Vijana au watoto wao walioamua kuacha matumizi
ya dawa za kulevya ili kuwalinda na vishawishi vinavyoweza kutoa nafasi ya kuwarejesha
tena kwenye matumizi ya Dawa hizo pamoja pombe haramu.
Mbunge wa
Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi ametoa wosia huo wakati wa kuwapokea
Vijana Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuacha kutumia Dawa za kulevya na
kupata mafunzo watakayoyatumia kuwasomesha wenzao kuachana na Dawa hizo hapo
katika Skuli ya Fujoni Wilaya ya Kaskazini “ B “.
Balozi Seif
ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema wapo Wazazi na
Familia Nchini ambao bado wanaendelea na tabia ya kuwatenga Vijana wao walioathirika
na Dawa za kulevya kwa kuchelea kufanyiwa matendo ya maudhi kama wizi.
Alisema
tabia hiyo inafaa kuachwa kwa vile kama haikutafutiwa ufumbuzi inaweza kuzalisha zaidi Vijana wanaotumbukia
katika matumizi ya Dawa za kulevya na hatimae kuwa na kundi kubwa la walevi ndani ya Jamii ambao ni nguvu kazi ya
Taifa.
Balozi Seif
alionyesha furaha yake kutokana na ujasiri
mkubwa ulioonyeshwa na vijana hao wa kuamuwa kuacha matumizi ya Dawa za
kulevya na kujitolea kuwa mfano kwa wenzao wenye tabia hiyo.
Aliwaomba Vijana
hao kuwa na hadhari ya kutokubali kudanganywa na baadhi ya watu hasa wanasiasa
ya kushawishiwa kujiingiza matika matendo maovu kama uvunjifu wa Amani.
Balozi Seif
alisema katika kipindi hichi cha Taifa kukaribia katika uchaguzi Mkuu Vijana
wana wajibu wa kupima kwanza chochote wanachoambiwa kabla ya kufikia uamuzi wa
kuchukuwa hatua.
Katika
kukabiliana na changamoto hizo Balozi Seif alifahamisha kwamba akili za kuambiwa
lazima vijana hao pamoja na Wananchi
wote wanapaswa kuzichanganya na zao ili
kupata maamuzi muwafaka.
Akiunga
mkono maamuzi ya Vijana pamoja na wazee wa Kijiji cha Fujoni katika juhudi za
kukaa pamoja na kutafuta mbinu za kukabiliana na matatizo ya matumizi ya Dawa
za kulevywa Kijijini hapo Balozi Seif aliahidi kuwapatia Boti ya Uvuvi na vifaa
vyake ili iwasaidie katika shughuli zao za kujiongezea ajira.
Balozi Seif
alieleza kwamba Mapato ya Boti hiyo pia wanaweza kuanzia jengo la Ofisi yao kwa
hatua ya ujenzi wa msingi na yeye atakuwa tayari kuongeza nguvu katika
kuwapatia vifaa ikiwemo matofali kwa ajili ya kuendeleza jengo lao.
Akitoa
Taarifa fupi Mwakilishi wa Umoja wa
kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na Pombe Tanzania
Bwana Abdulrahman Mohammed Abdulla
alisema Taasisi yao iliyoasisiwa mwaka 2009 tayari imeshafungua vituo Vinne vya
kutoa mafunzo kwa vijana walioamua kucha dawa za kulevya Bara na Zanzibar.
Bw.
Abdulrahman alisema vijana kati ya 56 na 65 wameshapatiwa mafunzo kwenye vituo
hivyo ambapo zaidi ya asilimia 35% ya Vijana waliopita kwenye vituo hivyo
wamerejea katika hali za kawaida na kufanya matumizi ya udungaji wa sindao
kupungua pia.
Alifahamisha
kwamba mafunzo hayo hulengwa zaidi katika kuwapatia Vijana hao ushauri nasaha
unaojumuisha uwepo kwa baadhi ya wazazi kwenye vituo hivyo, tiba pamoja na
huduma za michezo.
Mwakilishi
huyo wa Umoja wa kusaidia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya na
Pombe Tanzania alifahamisha kwamba zipo baadhi ya changomoto zinazokwamisha
utekelezaji na malengo ya taasisi hiyo.
Alitaja
baadhi changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa huduma rafiki katika Vituo
vya Afya jambo ambalo huwakatisha tamaa Vijana walioamua kuacha matumizi ya
Dawa za kulevya na kurejea tena baada ya kukosa usimamizi mzuri.
Mapema Sheha
wa Shehia ya Fujoni Bwana Said Mgeni Bakari alisema Wananchi wa Kijiji cha
Fujoni waliadhimia kusimamia mapambano dhidi ya matumizi ya Dawa za kulevya
ndani ya Kijiji hicho.
Sheha Said
alisema dhamira hiyo ndiyo iliyoibua kuanzishwa kwa Kikundi shirikishi na
Polisi jamii kwa lengo la kukabiliana na wimbi la vitendo hivyo vya matumizi
pamoja na uuzaji wa Dawa za kulevya na Pombe ndani ya Kijiji hicho.
Alifahamisha
kwamba licha ya juhudi zilizochukuliwa na Wananchi hao lakini bado lipo tatizo
la ukosefu wa vifaa vya kufanyia kazi pamoja na Ofisi kwa Kikundi hicho cha Polisi
Jamii na ulinzi shirikishi Fujoni.
Vijana hao
Sita wa Kijiji cha Fujoni walioamua kuachana na matumizi ya Dawa za Kulevya
walipatiwa mafunzo ya Miezi sita katika Nyumba ya kurekebishia Tabia kwa watu
walioamua kuacha Matumizi ya Dawa za Kulevya ya Mombasa nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Wakati huo
huo Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope Balozi Seif ameukabidhi Uongozi wa Mamlaka
ya Maji Zanzibar { ZAWA } shilingi Milioni 5,000,000/- kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Kibanda
cha Maji katika Kijiji cha Kinduni.
Ujenzi wa
Kibanda hicho una lengo la kuimarisha miundo mbinu ya upatikanaji wa huduma za
Maji safi na Salama ndani ya Kijiji hicho chenye changamaoto ya upatikanaji wa
huduma hiyo muhimu.
Balozi Seif
aliushukuru Uongozi mzima wa Mamlaka ya Maji Zanzibar kwa hujudi uliochukuwa wa
kushirikiana na ule wa Jimbo la Kitope katika kuwaondoshea usumbufu wa huduma
ya maji safi na salama wananchi wa jimbo hilo.
Alisema
juhudi hizo kwa kiasi kikubwa zimechangia kutatua changamoto za upatikanaji wa
huduma ya maji katika Vijiji vingi vilivyomo ndani ya Jimbo la Kitope.
Akipokea
fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha
ujenzi wa Kibanda cha Maji Kinduni Mkurugenzi
Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Zanzibar { ZAWA } Dr. Mustafa Garu alisema miradi
mingi ya Maji iliyoanzishwa na Mamlaka hiyo inatekelezwa ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma ya Maji Wananchi walio
wengi Nchini.
Dr. Garu
aliutaja mradi wa Maji uliopata Mkopo kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika uko
tayari kufanya kazi na utakuwa ukihudumia kwenye maeneo mengi ya Mji wa
Zanzibar.
Hata hivyo
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Mamlaka ya Maji Zanzibar aliwahakikishia Wananchi
kwamba Mamlaka hiyo itafanya juhudi ya kuwapatia huduma za maji wananchi
wakaondelea kuwa na uhaba wa huduma hiyo katika kipindi kinachoingia cha Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani.
Alisema ule
mpango wa kusambaza huduma za maji Mjini
na Baadhi ya Vijiji vyenye upungufu wa huduma hiyo kwa kutumia Magari maalum ya
kusambazia maji utaendelea kutekelezwa ili kuwapa fursa Wananchi kupata muda wa
kufanya mambo mengine ya Kimaisha.