Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar { BTMZ } Sharifa
Khamis akitoa maelezo wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa vifaa vya michezo kwa
Viongozi na wachezaji wa mchezo wa Kikapu Zanzibar Ofisini kwa Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi. Picha
na Hassan Issa–OPMR
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni Utalii na Michezo Dr. Ali
Saleh Mwinyikai akizungumzia mafanikio ya Wizara hiyo katika kuimarisha sekta
ya michezo ndani ya miaka Mitano iliyofikia utekelezaji wake kwa asilimia 98%.Picha
na HassanIssa–OPMR
Balozi Seif akizungumza na Viongozi a Wanamichezo wa mchezo wa Kikapu
Zanzibar katika hafla ya kukabidhiwa vifaa vya michezo vilivyotolewa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein. Picha
na Hassan Issa–OPMR
Balozi Seif akimkabidhi vifaa vya Michezo Kiongozi wa Timu ya Mpira wa Kikapu
ya Wanawake ya Jeshi la Wananchi wa
Tanzania Birigedia Nyuki Hidaya Khamis.
Picha na Hassan Issa–OPMR
Picha na Hassan Issa–OPMR
Kiongozi wa Timu ya Mpira wa Kikapu ya Stone Town Ali Shebe
akipokea vifaa vya michezo kwa ajili ya timu yake kutoka kwa Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif. Picha
na Hassan Issa–OPMR
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Zanzibar
Ramadhan akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Viongozi na wachezaji wenzake
mara baada ya kupokea vifaa vya michezo kutoka kwa Balozi Seif vilivyotolewa na
Rais wa Zanzibar Dr. Shein.
Picha na Hassan Issa–OPMR
Picha na Hassan Issa–OPMR
Press Release
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameupongeza Uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni,
Utalii na Michezo Zanzibar kwa kazi kubwa
unayoifanya katika kuendeleza sekta ya michezo hapa Nchini.
Alisema
Wizara hiyo imesimamia vyema katika kurejesha michezo mingi kwenye ukawaida
wake tokea mwaka 2010 na kuiomba isimamie pia kuurejesha mchezo wa Vinyoya {
BEDMINTON } ambao umeiletea sifa kubwa Zanzibar Kimataifa katika miaka ya
nyuma.
Balozi Seif
alitoa pongezi hizo wakati akikabidhi vifaa vya michezo kwa Timu 10 za Waume na
Tano za Wanawake za Mchezo wa Vikapu { Basketball } vilivyotolewa msaada na
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein.
Vifaa hivyo
alivyovikabidhi kwa Viongozi na wanamichezo hao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini
Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar ni pamoja na Seti za Jezi,mipira, Viatu
pamoja na soksi.
Balozi Seif
aliwaeleza Viongozi na Wanamichezo hao wa Mchezo wa Kikapu kwamba Michezo mingi
imerejea katika uhalisia wake kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM ya
mwaka 2010 iliyotilia mkazo uimarishaji wa Sekta ya Michezo Nchini.
Alifahamisha
kwamba Zanzibar ilibahatika kuwa na aina mbali mbali ya Michezo tokea katika
miaka ya 50 na baadhi yao kufifia katika
miaka ya 80 na 90 jambo ambalo limechangia kuporomoka kwa umaarufu wake katika
Nyanja ya michezo Kimataifa.
“ Yale mambo
ya michezo hivi sasa yanaonekana kurejea kutokana na kutiliwa mkazo ndani ya
Ilani na Sera ya Chama Tawala cha CCM ya Mwaka 2010 “ . Alisema Balozi Seif.
Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar waliwapongeza Viongozi wa Mchezo wa Kikapu
Zanzibar kwa umahiri wao wa kuendeleza
mchezo huo uliokuwa maarufu ndani ya
Bara la Amerika.
Alisema
mchezo wa Kikapu hivi sasa umekuwa maarufu hapa Nchini unaoonekana kutabiriwa
kuwa na wachezaji maarufu wanaoelekea kuwa kama akina Jordan
wa Marekani.
Balozi Seif
alisisitiza kwamba katika kuhakikisha sekta ya michezo inaendelea kuimarika
alisema Serikali kwa upande wake itajitahidi kutafuta mbinu na wafadhili wa
kusaidia mafunzo sambambana na walimu wa
michezo tofauti.
Mapema
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Dr. Ali Saleh
Mwinyikai alisema miongozo ya kazi iliyokabidhiwa Wizara hiyo kupitia Dira ya
Ilani ya Mwaka 2010 ndio iliyopelekea mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta
ya michezo hapa Zanzibar.
Dr.
Mwinyikai alisema kwamba utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Habari,
Utamaduni, Utalii na Michezo katika kuimarisha Sekta ya Michezo umefikia zaidi
ya asilimia 98% ya lengo lililokusudiwa kwa kuungwa mkono na Serikali Kuu.
Naye
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar {BTMZ } Sharifa Khamis
alisema bado sekta ya michezo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi zinazosababisha
kudumaza kwa baadhi ya michezo Nchini.
Mwenyekiti
Sharifa alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ukosefu wa vifaa vya
michezo, miundo mbinu mibovu ya sekta hiyo hasa kwenye viwanja, Ufinyu wa
mafunzo pamoja na ukosefu wa mashindano ya Kimataifa ya mechi za Kirafiki kwa
timu za Zanzibar.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya Viongozi wa wanamichezo hao Makamu Mwenyekiti wa Chama
cha Mpira wa Vikapu Zanzibar Ramadhan Khamis amemshukuru Rais wa Zanzibar
pamoja na Balozi Seif kwa juhudi zao wanazozichukuwa katika kuunga mkono sekta
ya Michezo Nchini.
Ramadhan
alisema juhudi za viongozi hao wa Kitaifa ndizo zilizopelekea na kuchangia kwa
kuibuka kwa Vipaji vya wanamichezo katika michezo tofauti pamoja na Zanzibar
kujiwekea rikodi nzuri za ushindi katika mashindano ya Kimataifa.
Makamu
Mwenyekiti huyo wa Basketball Zanzibar alieleza kwamba wanamichezo hao
wataendelea kuwaunga mkono Viongozi hao katika kuhakikisha kwamba wanafanikiwa
katika kutekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi wote.